FAIDA ZA MADINI YA FLOURIDI (FLOURIDE)

Flouridi ni madini ambayo kiasili hupatikana katika vyakula vingi na maji. Flouridi huungana na madini mengine katika meno na kutengeneza tabaka la enameli(tabaka la juu kabisa la meno) ambalo ni imara na sugu zaidi kwa tindikali ambayo husababisha meno kutoboka.
Tindikali hii katika meno huaribu tabaka la enameli kwa mchakato ambao kitaalamu huitwa "demineralization". Mchakato huu huanza kwa kudhoofisha tabaka la enameli na kupelekea kuanza kutengenezwa kwa mashimo madogo katika meno na inaweza kuendelea na kutengeneza mashimo makubwa zaidi na mwishoni hata kupoteza meno. Hatua za mwanzo za mchakato huu wa "demineralization" zinaweza kuzuiwa kwa kuweka madini ya flouride katika meno.
Kuna njia mbili ambazo madini ya flouridi hulinda tabaka la enameli katika meno ambazo ni;
- Kimfumo
- Kwa njia ya kuweka moja kwa moja kwenye meno
Madini ya Flouridi yanaweza kupatikana kwa kuyatumia moja kwa moja kutoka kwenye dawa za meno na dawa za kusukutua na mara chache inaweza kupakwa kwenye meno na daktari wa meno ambayo huwa katika kiwango kikubwa.
Ukiwa unatumia dawa za meno zenye madini ya flouridi unaweza kusaidia kuzuia meno kutoboka pale ambapo tindikali inakua imeishambulia meno. Mate huwa yana kiwango kidogo cha madini ya flouridi, hivyo basi kwa kutumia dawa za meno zenye madini ya flouridi huongeza kiwango cha madini ya floridi kwenye mate ambayo kiasili hufanya usafi wa meno.
![]() |
| Baadhi ya bidhaa zenye madini ya flouridi |
Ni muhimu kusafisha meno kwa kutumia dawa za meno zenye flouridi kwani imethibitishwa kisayansi kuwa madini ya flouridi husaidia kuzuia meno kutoboka. Dawa zenye madini ya flouridi zinatakiwa kutumika katika maisha yote. Kwa watoto hakikisha wanatumia dawa za meno zenye kiwango kidogo cha flouridi mpaka pale wanapokua wanauwezo wa kutema dawa wakati wa kupiga mswaki.

Comments
Post a Comment