AFYA NA USAFI WA KINYWA KWA WATOTO
Afya njema ya mtoto ni jukumu la mzazi, afya ya kinywa ni kati ya sehemu muhimu ya afya ya mtoto kwa ujumla. Matunzo ya meno na fizi za mtoto huanza na mzazi mwenyewe. Matunzo mazuri ya meno kwa watoto huwasaidia kuwa na afya njema ya kinywa baadae na hupunguza nafasi ya kupata magonjwa ya kinywa wakiwa wakubwa kwa kuwa wanakuwa wametengenezewa mazingira, uwezo na ufahamu wa jinsi ya kutunza meno na umuhimu wa kufanya hivyo.
Usafi wa Kinywa kwa Watoto Wachanga.
Watoto huzaliwa meno yakiwa tayari yamekwisha tengenezwa lakini huwezi kuyaona kwa sababu yanakua ndani ya fizi. Meno huanza kujitokeza nje ya fizi mtoto akiwa na umri kuanzia miezi 6 lakini ni vizuri kuanza usafi wa kinywa kwa mtoto hata kabla meno hayajaanza kutoka kwani "kwenye fizi safi na zenye afya huja meno safi na yenye afya".
- Futa fizi za mtoto kwa kitambaa safi kila baada ya kumlisha, hii husaidia kuondoa bakteria wanaosababisha meno kuoza.
- Pale meno yanapoanza kuota, hakikisha unaanza kumpigisha mswaki kwa kutumia mswaki laini na dawa ya meno yenye flouride kwa kiwango cha watoto.
- Ondoa chupa ya maziwa pale mtoto anapomaliza kunywa ili kuzuia kuoza kwa meno kunakosabishwa na maziwa, "baby bottle tooth decay".
- Hakikisha unapanga miadi "appointment" na daktari wa meno pale mtoto anapoanza kuota meno ya kwanza hii husaidia matunzo ya meno na mazoea mazuri ya mtoto katika mazingira ya matibabu ya meno.
Kwa watoto kuanzia miaka mitatu, yafuatayo ni mambo ya kuzingatia;
- Hakikisha anapiga mswaki kwa dawa ya meno yenye flouride kwa kiwango cha watoto
- Hakikisha anapiga mswaki mara mbili kwa siku, asubuhi na usiku kabla ya kulala
- Anza mazoea ya kumfundisha kufloss
- Kuonana na daktari wa meno kila baada ya miezi sita
Usafi wa Kinywa kwa Watoto Kuanzia miaka Saba
- Watoto katika umri huu wanakua makini muonekano wao, ni vizuri kuwakumbusha kuwa usafi wa meno na kinywa utasaidia kuwafanya waonekane vizuri zaidi.
- Wakumbushe watoto kupiga mswaki na dawa ya meno yenye flouride mara mbili kwa siku ili kuzuia meno kutoboka
- Hakikisha wanavaa vifaa vya kulinda meno yao wakiwa wanafanya michezo ili kuzuia meno kuvunjika wanapokua wameanguka au kupata ajali wakiwa michezoni
- Hakikisha watoto wanaonana na daktari wa meno kila baada ya miezi sita ili kuhakikisha kila kitu kipo sawa.
AFYA NJEMA NA UKUAJI MZURI WA MTOTO HUTEGEMEA LISHE BORA NA MUHIMU ZAIDI AFYA BORA YA KINYWA AMBAYO NDIO SEHEMU CHAKULA HUPITIA. AFYA BORA YA KINYWA NI AFYA BORA YA MWILI MZIMA.
Comments
Post a Comment