AFYA YA KINYWA NA MENO KWA WAJAWAZITO
Ujauzito ni kipindi ambacho mwanamke anakua ana mahitaji mengi na mabadiliko mengi katika mwili na baadhi ya mabadiliko hayo yana athari kwa afya ya kinywa na meno kama hakutakua na uangalizi mzuri wa kinywa na meno kwa kipindi cha ujauzito.
Moja ya matatizo ya kinywa na meno yanayowapata wajawazito wengi ni tatizo la fizi kuvimba na kutoa damu ambayo kitaalamu inaitwa "pregnancy gingivitis au pregnancy tumour".
Tatizo hili husababishwa na kuongezeka kwa kiwango cha homoni iitwayo "progesterone" ambayo huchangia kuongezeka kwa mtirirko wa damu kwenye fizi na kuzifanya ziwe sensitive, kuvimba na rahisi kutoa damu wakati wa kupiga mswaki. Mabadiliko ya kiwango cha homoni hii pia huwapa urahisi bakteria ambao husababisha magonjwa ya fizi kukua na kusababisha magonjwa ya fizi.
Tatizo hili la fizi linaweza kutokea muda wowote kuanzia mwezi wa pili mpaka wa nane lakini huwa kwa kasi sana katika kipindi cha pili cha ujauzito (second trimester) kuanzia mwezi wa tatu mpaka wa sita.
| Pregnancy gingivitis |
Kuna umuhimu gani wa kutibu magonjwa ya fizi kwa wajawazito?
Matibabu ya magonjwa ya fizi kwa wajawazito ni muhimu sana kabla hayajakua na kufikia hali mbaya ambayo inaweza kupelekea meno kutoka au kutolewa. Afya ya mama mjamzito na afya ya mtoto inaweza kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na afya ya kinywa na meno hasa tatizo hili la fizi kwa sababu wakati huu mama mjamzito huwa anapata tabu sana kwenye kula hii hupelekea afya yake kuzorota na ya mtoto pia. Tafiti nyingi zinaonesha kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya matatizo ya fizi na meno na kuzaliwa kwa watoto njiti (premature delivery).
Nini kifanyike ili kuepuka matatizo ya fizi wakati wa ujauzito?
Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia ili kuhakikisha una afya nzuri ya kinywa na meno kwa kipindi chote cha ujauzito.
- Hakikisha unamuona daktari wa meno mara kwa mara ili kuhakikisha hakuna tatizo lolote la meno na kama lipo basi linashughulikiwa mapema iwezekanavyo.
- Tumia mswaki wenye brush laini na kupiga mswaki taratibu ili kuepusha kuziumiza fizi ambazo kwa wakati huo zinaweza kutoa damu kwa urahisi.
- Tumia dawa ya meno yenye madini ya flouride kwa kupiga mswaki mara mbili kwa siku
- Hakikisha unasukutua mdomo kwa dawa ya kusukutua na pia kila unapopata hali ya kutapika ili kuepusha tindikali itokayo tumboni kubaki kwenye meno na kusababisha meno kutoboka.
- Kula chakula bora chenye uwingi wa madini ya calcium na phosphorus, protini na vitamini A C na D.
AFYA YA KINYWA NA MENO KWA MAMA MJAMZITO NI MUHIMU KWA AFYA YAKE NA AFYA YA MTOTO PIA.
Comments
Post a Comment