MENO
Meno ni viungo vya mwili vilivyopo kinywani vyenye kazi ya kutafuna yaani kumega chakula kama maandalizi ya kukimeza na kumeng'enya.
Meno hupatikana kwa wanyama wenye uti wa mgongo. Nje ya kutafuna chakula hutumiwa pia
kama silaha za kujilinda au kushambulia wanyama wengine. Wanyama kadhaa
huwa na meno nje ya mdomo kwa matumizi kama silaha (mfano: tembo) yanayoweza kutumiwa pia kama vifaa vya kuchimba (mfano: nguruwe mwitu).
Kwa binadamu meno hupatika kinywani tu. Kazi kubwa ya meno kwa binadamu ni katika umeng'enyaji wa chakula
anachokula na mara chache watu hutumia katika kusaidia kukata vitu mbalimbali kama
kutatua kitambaa au kukata kamba au waya ingawa kufanya hivyo kunaweza kuwa na madhara kwa meno. Binadamu ana aina mbalimbali
za meno zinazomsadia kula vyakula vya aina mbalimbali kama vile vya
mimea na nyama. Kwa kawaida mtu mzima huwa na meno thelathini na mbili.
Binadamu huwa na aina mbili za meno. Tunazaliwa na mbegu za meno ya
utoto yanayobadilishwa wakati wa kubalehe kwa meno ya kudumu. Kwa hiyo
kuna wakaa mbili za meno.
Idadi ya meno ya utoto katika wakaa ya kwanza ni 20. Huanza kuota mtoto anapokuwa na umri wa miezi sita na kawaida yote huwa yamekwisha kuota mtoto anapotimiza umri wa miaka miwili.
Idadi ya meno katika wakaa ya pili ni 32. Huanza kuota katika umri wa
miaka sita, yakakamilika katika umri wa miaka 18-20. Lakini mwingine
huota upesi au hukawia.
Meno ya kudumu.
Meno ya watoto.
AINA ZA MENO
Umbo la meno hufuatana na kazi ambayo inayapasa kufanya. Meno yaliyopo katikati ya kila taya huwa na kingo kali za kukatia chakula. Haya huitwa meno ya kukatia au meno ya mbele (incisors). (meno 8 ya kukatia, katika kila taya yapo meno 4).
Meno yanayofuata meno ya kukatia ni machonge (canine teeth). Yapo machonge 4 kwa ujumla; katika kila taya kuna machonge 2. Kazi yao ni kurarua chakula.
Meno yanayofuata machonge huitwa magego madogo (premolars) (jumla ya magego madogo ni 8; na katika kila taya yapo 4); na meno yanayoyafuata hayo huitwa magego
(molars) (magego yote ni 12, na katika kila taya kuna magego 6. Magego
madogo na magego ni kwa kusagia chakula. Katika meno ya watoto huwa
hakuna magego madogo.
MUUNDO WA JINO
Meno hukaa kwa uthabiti ndani ya vitundu vya mataya. Kila jino lina sehemu mbalimbali. Sehemu ambayo huonekana kinywani ni kichwa cha jino (tajino), na sehemu iliyomo ndani ya taya ni mzizi wa jino.
Sehemu kubwa ya jino ni mfupa laini unaoitwa dentini. Dentini kwenye sehemu ya tajino au kichwa hufunikwa kwa gamba la jino. Kichwa ni cha ufupa mgumu sana wenye rangi nyeupe ya kung’aa unaoitwa enameli ya jino. Kazi yake ni kulinda mfupa laini zaidi ya ndani. Pembe ya shina hulindwa na tabaka aina ya saruji ijulikanayo kwa jina la kitaalamu kama sementi ya jino (ing. cementum).
Katikati hasa ya sementi ya jino na mfupa wa taya kuna utando, ambao unasaidia kukuza jino katika kitundu chake, nao (utando huo) hulingana na ufizi wa meno.
Ndani ya jino kuna uwazi mwenye tishu ya neva na mishipa ya damu. Neva pamoja na mishipa ya damu huingia katika mvungu penye ncha ya kizizi cha jino.


Comments
Post a Comment